KUDORORA KWA KISWAHILI NCHINI

Hujambo?

Ninaomba kuichukua nafasi hii kwanza kabisa kuwapongeza ndugu Bitugi Matundura kwa makala yake ya 'Asili ya Kudorora kwa Kiswahili' na Milkah Righa kwa makala yake ya 'Barua kwa Washikadau wa Kiswahili Nchini' ya 06-01-2012.
Pili, ni kuwaunga mkono na kujibu baadhi ya maswali mazito yaliyoulizwa na ndugu Milkah Righa. Kudorora kwa Kswahili kote nchini na haswa shuleni, kunachangiwa na mambo mengi. Miongi mwa mambo hayo ni vitabu vya kiada vinavyotumiwa. Ni wazi kuwa Taasisi ya Elimu nchini, imeidhinisha vitabu vingi vinavyotumiwa shuleni. Vitabu vyenyewe vimeandikwa na waandishi mbalimbli ambao wana mitazamo mbalimbali inayokinzana kuhusu kile ambacho wamekiandika. Mifano mizuri ni kuhusu Ngeli za Kiswahili tunazoambiwa kuwa ndio uti wa mgongo wa lugha ya Kiswahili. Waandishi wengi hawana msimamo mmoja wa namna wanavyozianisha na kuzichambua ngeli za Kiswahili.Mathalan, ngeli za A-WA, I-ZI na I-I. Vitabu vingine vinasema kuwa nomino sukari, chumvi,asali, mvua na damu ni ngeli ya I-ZI ilhali vingine vinasema ni I-I. Nomino maiti kwa wengine ni ngeli ya I-ZI huku waandishi wengine wakisema ni A-WA. Mfano wa pili, ni Sauti za Kiswahili katika shule za upili. Mwandishi anaeleza anachokifahamu yeye tofauti na alichoeleza mwandishi mwenzake. Mfano wa tatu, ni kuhusu Uchanganuzi wa Sentensi;kipengele katika kidato  cha tatu. Hapa vile vile uchanganuzi umetofautiana pakubwa.

Mfano mwingine ni katika kipengele cha insha. Kipengele hiki hutumiwa kama kigezo cha kutambua usanifu wa lugha ya mtahiniwa na namna anavyoimudu. Ajabu ni kwamba, licha ya kipengele hiki kuwa na uzito wake, kungali na vitabu ambavyo vinakanganya na kuchanganya wanaojifunza Kiswahili. Baadhi ya vitabu vinatoa miundo tofauti ya kuandika insha za Barua,Ripoti, Kumbukumbu, Hotuba na Methali. Vinakuwa vigumu kumwambia au kumshauri mwalimu ama mwanafunzi kutumia vitabu bora hususan inapozingatiwa kuwa vitabu vyote hivyo vina alama ya kuthibitisha kuidhinishwa na Taasisis ya Elimu.

Jambo jingine, ni wanahabari. Ni wazi kuwa kila mmoja katika jamii tunazoishi, huamini sana vyombo vya habari kwa kile ambacho kitasemwa na mwanahabari. Kuna baadhi ya wanahabari ambao hushiriki katika vipindi vya Kiswahili. Lakini wanapotoka katika kipindi hicho, huanza kutumia lugha isiyoeleweka na ambayo inakusudia kuvunja na kuharibu Kiswahili. Isitoshe, zipo stesheni ambazo kwazo hakuna lugha nyingine inayotumiwa ila lugha ya mtaani maarufu kama Sheng`. Hata matangazo mengine ya biashara yana misamiati ya lugha hii. Vipindi vya humu nchini kwenye runinga zetu vimenuia kuwachekesha watazamaji na wasikilizaji kwa lugha ya Sheng`. Waigizaji katika vipindi hivyo wamekusudia kuvunja na kuvyoga Kiswahili hadharani bila kuhofia chochote na yeyote. Kwa mfano ni nani asiyejua kuwa ni makosa wala haifai mtu kusema 'Mtoto changu au Kiti yule?'. Ni nini iwapo huku si kunuia kuharibu Kiswahili hadharani? Watoto huiga kwa kusema hivyo na kuandika hivyo. Halafu tutarajie matokeo ya Kiswahili kuwa shwari?

Kenya,nchi ambayo ilijinyakulia uhuru mwaka wa 1963 kwa msaada mkubwa wa Kiswahili, ingali na gazeti moja kwa lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha rasmi na ya taifa. Majarida yote yaliyotapakaa mijini, yanameremeta kwa lugha ya Kiingereza au lugha za kiasili. Bila shaka matokeo ya Kiswahili hayawezi kuwa ya kuvutia.

Shule zetu zinamilikiwa au zinasimamiwa na watu au walimu walio na mielekeo hasi dhidi ya Kiswahili. Siku ya kutumia Kiswahili shuleni ni moja tu kwa juma. Kiswahili chenyewe huwa cha kubahatisha na cha kujilazimisha. Siku nyingine zote,huwa ni Kingereza.

Imani tuliyonayo finyu na dhaifu ni kuwa mtu anayezungumza Kingereza ndiye anayeonekana msomi zaidi kuliko wote bila kujua kwamba tunajidanyanya.Viongozi wetu hawawezi kutoa hotuba iliyoandikwa kwa Kiswahili kisha ile nyingine kwa Kingereza. Wanapotanguliza hotuba yao kwa Kingereza huona kama watu ambao wamefanya jambo kubwa na la msingi. Hawajiulizi kuwa ujumbe huo ulikuwa umemkusudia nani. Baadhi ya viongozi hupenda kutumia sheng huku wakidai kuw wanawalenga vijana. Kinachoshangaza ni kwamba hakuna kijna yeyote ambaye nimemsikia akidai kuhutubiwa kwa lugha hii kama wasemavyo viongozi hao. Kwa kufanya hivi inakuwa nadra kuimarisha Kiswahili.

Jambo la mwisho ni kuhusu sera ya lugha. Taifa letu kwa miaka na dahari limekosa sera ya lugha.Iwapo tutakuwa na sera ya lugha madhubuti na sote tuonyeshe ari, nia na ghera ya kujivunia Kiswahili, hatutawahi kulalamika kuhusu kudorora kwa Kiswhili nchini kila kunapokucha. Sisi sote ni washikadau wa Kiswahili. Tusiliwache dau hili kuzama na Kiswahili hakitadorora nchini. Kitabaki kusimama imara kama milima!

Comments

Popular posts from this blog

MIGUNA MIGUNA MITINI