MIGUNA MIGUNA MITINI

Hujambo?

Miezi michache iliyopita, wakenya na ulimwengu kwa jumla, walipokea habari kutoka kwa aliyekuwa mshauri mkuu wa Waziri Mkuu,Raila Odinga katika serikali ya muungano, bw. Miguna Miguna, kuwa alikuwa akikiandika kitabu kumhusu Raila Odinga.

Taarifa hizi zilijiri muda mfupi baada yake kupigwa kalamu. Wengi nikiwa mmoja wao, tulisubiri kwa hamu na ghamu kujua alichotaka kukisema bwana Miguna. Hakusikika kwa muda mrefu.

Baadaye aliibuka na kutangaza siku rasmi ya kukizindua kitabu chake. Kabla ya kukizindua rasmi, ujumbe uliokuwa ndani ya kitabu hicho chenye anwani Peeling Back The Mask, ulikuwa tayari katika vyombo vya habari.

Ilibainika wazi licha ya ujumbe huo kiduchu kuwa yaliyomo hayakuwa ya Mheshimiwa Raila Odinga tu. Pia waliomo na wasiokuwemo serikalini.

Siku ya ndovu kumla mwanawe ilikuwa imefika. Wa kualikwa wakaalikwa na wakususia wakafanya hivyo. Vinani! Bwana Miguna hakutishika. Alizindua kitabu chake mbele ya vyombo vya habari na ulimwengu kwa jumla. Wakati wa hotuba yake, wengi walicheka kwa namna alivyodhihirsha kuwa na siri kali za watu maarufu hapa Kenya na zaidi Raila Odinga. Alikashifu na kulaani uozo na uovu uliokithiri na kushaimiri miongoni mwa viongozi wa taifa tukufu la Kenya.

Kilichonishangaza zaidi ni pale aliposema hadhaarani kuwa hakukuwepo na kiongozi ambaye angemsaza kumfikisha katika mahakama ya uhalifu ya mataifa, Hague, Uholanzi iwapo angepewa fursa yakufanya hivyo. ( Every leader  here, I can take to the Hague). Kuzidisha msumari moto kwenye kidonda ni pale aliposema kwamba alikuwa na ithibati tosha kuhusu ghasia za siasa zilizokumba taifa la Kenya mwaka wa 2007/2008.

Alijipiga kifua na kuapa kutoogopa yeyote na chochote duniani. Hata kifo. Niliposikia hay binafsi, nilimwona mtu ambaye sijawahi kumwona duniani. Nilimwona jasiri, mkakamavu na mtu ambaye angeweza kuwaambia wa Wakenya ukweli wasiojua. Niliamini kila alichosema.

Lakini pindi tu kiongozi mkuu wa mashtaka wa Kenya bwana Keriako Tobiko aliposema bwana Miguna atoe taarifa aliyo nayo kuhusu ghasia za siasa na pia kutafutwa na askari, kimya kilitawala nchi. Maajabu ya Mussa ni pale habari zilipotufikia kuwa, Miguna Miguna hakuwa Kenya tena. Yeye pamoja na familia yake walisemekana kutorokea Canada. Kisa na maana? Alihofia uslama wake.

Swali ni je, ujasiri aliokuwa nao ulienda wapi? Iwapo alikuwa na taarifa kamili na ushahidi wa kutosha wa kile alichokisema, mbona akakimbia? Haya yatakuwa kama yale yaliyomkumba bwana John Githongo? Je, tupuuze aliyoyaandika na kuuona kama uongo mtupu ama tuamini? Je, atarudi Kenya hivi karibuni ama baada ya mambo kusahaulika kama ilivyo kawaida yetu? Ni nani aliyemshauri kuyanusuru maisha yake?

Bonface Andenga
Mtafsiri
Afrolingo 

Comments

Popular posts from this blog

KUDORORA KWA KISWAHILI NCHINI