MABADILIKO HAYAJI KWA KUWA VIGEUGEU!

Kila kunapokucha na kuchwa maisha yanazidi kuwa magumu na mazito ya kuweza kuyahimili na kustahimili. Bei ya bidhaa muhimu inaongezeka kwa kasi kama risasi. Anayebaki kulalamika na kunung`unika moyoni ni mwananchi wa kawaida. Iwapo atajaribu kuipaza sauti yake ili iwafikie washikadau, kilio chake huambulia patupu  kwa kupuuzwa na walalahai. Maskini wa Mungu anasalia kupiga dua ili siku moja iwe siku njema. Kufika kwa siku hii huwa ndoto ya alinacha. Kunabaki kuwa sawa na kutarajia kupata maji katika jangwa. Kila wanaposimama hawa walalahoi kuizungumzia hali hii, wanatoa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta kote ulimwenguni. Sababu ambayo wengine wanaiona kutokuwa ya msingi wowote na kuwaona wao kama wasaliti wa wananchi wao pindi tu wanapoyapata madaraka na mamlaka ya kunyanyasa.

Hata hivyo, huenda sisi ndisi waasisi wa baadhi ya matatizo yanayotutatiza. Tumekataa kuwa wakombozi wa taifa letu kwa sababu ya ubinafsi wetu. Mfano mzuri wa hali hii ni pale ambapo ilisemekana kwamba, mataifa kadhaa jirani ya Afrika Mashariki yananunua mafuta kwa bei nafuu kuliko Kenya ilhali mafuta yayo hayo yanapitia Kenya ndipo yafikie mataifa hayo mengine. Katibu Mkuu wa Mwungano wa Wafanyikazi pamoja na wengine, walijaribu kuomba kuwepo kwa mgomo wa matatu kulalamikia bei ghali ya mafuta na gharama ya maisha lakini hakuna yule ambaye alijaribu kuwasikiliza. Wengi haswa wahudumu wa matatu na wananchi walidai kuwa mgomo huo uliitishwa wakati mbaya. Kwa maana kwamba ulikuwa wakati wa watu kutafuta hela zaidi na kusafiri sehemu mbalimbali nchini. Kwa kugoma wangepoteza hela na kuharibu mambo mengi.

Huu ndio ninaosema ubinafsi tulionao. Tunasahau kuwa amani siku zote haiji ila kwa ncha ya upanga. Viongozi wetu hawawezi kufanya lolote kuyanusuru maisha ya wakenya mpaka pale wanaposikia vilio na kushuhudia migogmo kama njia pekee ya kudai haki halali. Na haki inapopatikana haiwi ya leo tu bali ya kesho na vizazi vijavyo. Tusisahau kuwa mabadiliko hayaji kwa kuwa VIGEUGEU!

Bonface Andenga
Rununu: 0728570252
Baruameme: andengaba@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

KUDORORA KWA KISWAHILI NCHINI

MIGUNA MIGUNA MITINI